Hifadhi ya Taifa Arusha, yenye ukubwa wa kilomita za mraba 328.4, iko umbali wa kilomita 62 (kiasi cha mwendo wa saa moja kwa gari) kutoka mji wa kitalii wa Arusha.
Hifadhi hii ina maeneo matatu muhimu: bonde la Ngurdoto (Ngurdoto Crater), maziwa ya Momella ambayo kila moja hutoa mandhari tofauti pamoja na Mlima Meru wenye urefu wa mita 4,566 (futi 14,990), hali ambayo inaifanya hifadhi kuwa na mazingira ya baridi.
Hifadhi ni maarufu kwa wanyama jamii ya tumbili wajulikanao kama mbega weusi na weupe. Wanyama wengine wanaopatikana kwa wingi katika hifadhi hii ni pamoja na twiga, pundamilia, nyati, tembo na digidigi. Aidha unaweza kuwaona chui wakibarizi katika vivuli vya matawi ya miti inayokingwa na maanguko ya maji huku makundi kadhaa ya batamaji yakitafuta wadudu katika maziwa ya Momella. Zaidi ya aina 400 za ndege wamethibitika kupatikana ndani ya hifadhi hii.
Safari za miguu na kupanda mlima Meru ni moja ya burudani muhimu katika hifadhi hii. Mpandaji anahitaji kati siku ya 3-4 za kupanda mlima. Zoezi hili ni muhimu kwa wale wanaotarajia kupanda Mlima Kilimanjaro.
Wakati mzuri wa kutembelea hifadhi hii ni kati ya mwezi Juni na Februari ingawa mvua inaweza kunyesha mwezi Novemba.
Kuna maeneo ya malazi ndani ya hifadhi yenye hadhi tofauti tofauti kama hoteli, nyumba za wageni na makambi ya kupiga mahema. Vilevile wageni wanaweza kupata malazi nje ya hifadhi katika miji midogo ya Usa River and Arusha Mjini