Hifadhi ya Taifa Gombe, ni ndogo kuliko zote nchini ikiwa na jumla ya kilomita za mraba 52 tu, lakini ina umaarufu mkubwa unaotokana na kuwa na wanyama aina ya Sokwe.
Gombe ni miongoni mwa makazi machache yaliyosalia ya Sokwe duniani. Ikiwa umbali wa kilomita 16 kaskazini mwa mji wa Kigoma, hifadhi hii ni ukanda mwembamba wa msitu wa mlimani unaokatizwa na miteremko mikali inayoingia katika mwambao wa Ziwa Tanganyika.
Hifadhi ya Taifa ya Gombe ilipata umaarufu duniani hasa baada ya mtafiti wa tabia za Sokwe duniani, Dk. Jane Goodall kufanya utafiti juu ya maisha na tabia za Sokwe wa Gombe kwa muda wa miaka 40 na kuandika vitabu kadhaa kuhusu viumbe hawa.
Wanyama wengine wanaopatikana katika hifadhi hii ni pamoja na kima wenye mikia myekundu na kima wa bluu. Wanyama wa jamii ya paka, kama chui na simba hawapo katika hifadhi hii na hivyo kuifanya kuwa salama kwa safari za miguu.
Unaweza kwenda katika hifadhi hii kwa ndege za abiria au za kukodi kutoka Dar es salaam hadi Kigoma mjini na baadaye kwa boti hadi Makao Makuu ya hifadhi. Kadhalika kuna huduma ya treni kutoka Mwanza na Dar es salaam pamoja na barabara itokayo Mwanza, Mbeya na Dar es Salaam.
Wakati mzuri wa kutembelea hifadhi hii ni wakati wa kiangazi, Julai-Oktoba kwani Sokwe hawapendi kutembea nyakati za mvua.
Sehemu za malazi katika hifadhi hii ni pamoja na hosteli, Kambi za mahema, nyumba za wageni na maeneo kadhaa ya kupiga kambi. Aidha wageni wanaweza kupata malazi mjini Kigoma.