Hifadhi ya Taifa Katavi, yenye ukubwa wa eneo la kilomita za mraba 4,471, iko juu ya uwanda mpana wa mafuriko Kusini Magharibi mwa Tanzania katika mkoa wa Rukwa.
Mandhari kuu katika hifadhi hii ni maeneo ya majimaji yenye majani, mimea mithili ya mitende pamoja na mto Katuma.
Hifadhi hii inasifika kwa idadi kubwa ya mamba na viboko nchini. Simba na chui waliopo katika hifadhi hii hawana shida ya mawindo: Katika himaya yao kuna makundi ya swala, nyamera, topi, pundamilia na nyati.
Kuna aina zipatazo 400 za ndege waliozagaa katika miti aina ya migunga, katika kingo za mto, mabwawa na makundi kadhaa ya mwari (pelicans) yanayoambaa ziwani. Ni kawaida kuyaona makundi makubwa ya tembo yakila majani katika mabwawa huku miili yao ikiwa imefunikwa na maji na magugu.
Hifadhi hii inafikika kwa ndege za kukodi na kwa gari kutoka Mbeya na pia kwa kupitia Kigoma (wakati wa kiangazi: Mei - Oktoba na kuanzia katikati ya Desemba hadi Februari). Inafikika pia kwa reli kutoka Dar es salaam kupitia Tabora hadi Mpanda na kwa gari toka Mpanda.
Kuna kambi za kitalil za kifahari, nyumba za wageni na maeneo ya kupiga kambi yaliyoko ndani ya hifadhi. Aidha, malazi ya hotel i yanaweza kupatikana mjini Mpanda, umbali wa kilomita 40.