Hifadhi ya Taifa Rubondo ni kisiwa kilichopo pembezoni mwa Ziwa Victoria, ziwa ambalo ni la pili kwa ukubwa duniani, likiwa linaziunganisha nchi tatu, Tanzania, Kenya na Uganda. Kikiundwa na mkusanyiko wa visiwa tisa vidogo vidogo.
Kisiwa cha Rubondo ni makazi na mazingira muafaka ya kuzaliana samaki wakiwemo sato na sangara. Sangara huweza kuwa wakubwa na kufikia uzito wa kilo hadi 100.
Hifadhi hii ina ukubwa wa kilomita za mraba 457 na iko kaskazini magharibi mwa Tanzania na inafikika kwa ndege za kukodi kutoka, Arusha, Ziwa Manyara, Serengeti na Mwanza; kwa njia ya barabara kutoka Mwanza - Sengerema - Geita - Nkome kisha kwa boti hadi hifadhini; kwa meli ndogo kutoka Muleba na Bukoba; vile vile kwa njia ya barabara kutoka wilaya ya Biharamulo na Muleba kupitia kijiji cha Mganza.
Fukwe za kisiwa hiki ni miongoni mwa makazi ya pongo na nzohe.
Aidha Hifadhi hii ni maskani makuu ya ndege wala samaki kama zumbuli (Kingfisher), chechele (Flycatcher) na taisamaki (Fish eagle).
Mbali na ndege hao kisiwa hiki ni makazi ya aina nyingine nyingi ya ndege wa majini na mimea kadhaa wa kadhaa ambayo hutoa harufa nzuri ya kuvutia. Wanyama wakazi wa hifadhi hii kama viboko, pongo, nzohe, fisi maji, mamba na pimbi wanashirikiana makazi na wanyama walio-hamishiwa katika hifadhi hii kama sokwe, tembo, mbega weusi na weupe na twiga.
Shughuli za utalii katika hifadhi hii ni pamoja na safari za miguu msituni, safari za boti na uvuvi wakutumia ndoano.
Wakati mzuri wa kutembelea Hifadhi hii ni wa kiangazi, Juni - Agosti. Aidha, wakati wa masika, Novemba hadi Machi (kwa ajili ya kuona maua na vipepeo) na vilevile Desemba - Februari (kwa kuwaona ndege wahamiaji).
Kuna kambi ya kifahari, nyumba za kulala wageni na maeneo kadhaa ya kupiga kambi kwa ajili ya malazi.