Hifadhi ya Taifa Saadani ina ukubwa wa kilomita zamraba 1,062. Hifadhi hii iko ufukweni mwa Bahari ya Hindi na ni hifadhi pekee Afrika Mashariki inayounganika na bahari.
Saadani iko umbali wa Kilometa 100 Kaskazini Magharibi mwa Dar es Salaam na umbali kama huo Kusini Magharibi mwa bandari ya Tanga.
Saadani inasifika kwa kuwa na wanyama kama tembo, twiga mbogo, ngiri, kuro, simba, chui, fisi na aina mbalimbali ya swala pamoja na Tumbili na ngedere.
Hifadhi hii ilianzishwa kama pori la akiba mwaka 1960 na ilitangazwa rasmi kuwa hifadhi ya Taifa mwaka 2005.
Wapo pia ndege mbalimbali kama vile Korongo wadogo “flamingo”. Hifadhi hii hutoa nafasi kwa wageni kuona wanyama pamoja na kuogelea baharini-muunganiko ambao ni wa kipekee kabisa Afrika Mashariki.
Unaweza kufika katika hifadhi hii wakati wowote wa mwaka, hata hivyo wakati wa mvua, Aprili na Mei barabara zinaweza zisipitike kwa urahisi.
Kwa kuangalia wanyama, kipindi cha Januari, Februari, Juni hadi Agosti ndicho kipindi kizuri zaidi.
Kuna kambi ya mahema, nyumba za kulala wageni, na kambi za kifahari kwa ajili ya malazi kwa wageni.